Part 21

 

46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake. 

47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri. 

48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wavunjifu. 

49. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu. 

50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu. 

51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao amini. 

52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri. 

53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa ghafla, na hali wao hawana khabari. 

54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa hakika imewazunguka makafiri! 

55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda! 

56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu. 

57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu. 

58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao, 

59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. 

60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. 

61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa? 

62. Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. 

63. Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu. 

64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua! 

65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha. 

66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua! 

67. Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za Mwenyezi Mungu wanazikataa? 

68. Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri? 

69. Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema. 

 

30 - AR-RUM

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) 

2. Warumi wameshindwa, 

3. Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda 

4. Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi. 

5. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

6. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui. 

7. Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera. 

8. Je! Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi. 

9. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao. 

10. Kisha ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara. 

11. Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake. 

12. Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa. 

13. Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao. 

14. Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika. 

15. Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika Bustani. 

16. Na ama walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu. 

17. Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na asubuhi, 

18. Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na adhuhuri. 

19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa. 

20. Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote. 

21. Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. 

22. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi. 

23. Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao sikia. 

24. Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao zingatia. 

25. Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi. 

26. Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii Yeye. 

27. Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 

28. Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo ogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili. 

29. Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru. 

30. Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui. 

31. Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina. 

32. Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho. 

33. Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao wametubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao Mlezi, 

34. Kwa kuyakataa tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua! 

35. Au tumewateremshia hoja ambayo kwayo ndio wanafanya ushirikina? 

36. Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na ukiwasibu uovu kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa. 

37. Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini. 

38. Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa. 

39. Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa. 

40. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha akakuruzukuni, kisha anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote katika hao mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika, na ametukuka na hayo mnayo mshirikisha naye. 

41. Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu. 

42. Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa walio tangulia. Wengi wao walikuwa washirikina. 

43. Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana. 

44. Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao. 

45. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri. 

46. Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema, na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru. 

47. Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya ukosefu. Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini. 

48. Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika waja wake, mara hao huwa na furaha. 

49. Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa. 

50. Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyo ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya shaka Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. 

51. Na tunge utuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya hayo wange endelea kukufuru. 

52. Kwani wewe hakika huwafanyi maiti wakasikia, wala viziwi wakasikia wito wakisha geuka kukupa mgongo. 

53. Wala wewe huwaongoi vipofu na upotovu wao. Huwasikilizishi ila wanao ziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walio nyenyekea. 

54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza. 

55. Na siku itapo simama Saa wakosefu wataapa kwamba hawakukaa duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyo kuwa wakipotozwa.  

56. Na walio pewa ilimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamuijui. 

57. Basi Siku hiyo hautawafaa walio dhulumu udhuru wao, wala haitotakiwa toba yao. 

58. Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur'ani. Na ukiwaletea Ishara yoyote hapana shaka walio kufuru watasema: Nyinyi si chochote ila ni waongo. 

59. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga muhuri kwenye nyoyo za wasio jua. 

60. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala wasikupaparishe hao wasio kuwa na yakini. 

 

31 - LUQMAN

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) 

2. Hizi ni Aya za Kitabu chenye hikima. 

3. Kuwa ni Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema, 

4. Wanao shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na Akhera. 

5. Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio wenye kufanikiwa. 

6. Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha. 

7. Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu. 

8. Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa nazo Bustani za neema. 

9. Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 

10. Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna. 

11. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri. 

12. Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa. 

13. Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa. 

14. Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio. 

15. Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda. 

16. Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote. 

17. Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.. 

18. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. 

19. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda. 

20. Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru. 

21. Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao? 

22. Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu. 

23. Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. 

24. Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu. 

25. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui. 

26. Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa. 

27. Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 

28. Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. 

29. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi? Vyote hivyo vinakwenda mpaka wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. 

30. Hivi ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na hakika wanacho kiomba ni cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtukufu na ndiye Mkubwa. 

31. Kwani huoni kwamba marikebu hupita baharini zikichukua neema za Mwenyezi Mungu, ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru. 

32. Na wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao huenda mwendo wa sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri mkubwa. 

33. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu mdanganyifu. 

34. Hakika kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anaye iteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari. 

 

32 - ASSAJDAH

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) 

2. Huu ni mteremsho wa Kitabu kisicho kuwa na shaka yoyote kinacho toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

3. Au wanasema: Amekizua? Bali hichi ni Kweli iliyo toka kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio fikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda wakaongoka. 

4. Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa siku sita, na akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki? 

5. Anapitisha mambo yote yalio baina mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyo hisabu nyinyi. 

6. Huyu ndiye Mwenye kuyajua yasiyo onekana na yanayo onekana. Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. 

7. Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo. 

8. Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu. 

9. Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru. 

10. Nao husema: Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi. 

11. Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi. 

12. Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa. 

13. Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu : Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu. 

14. Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda. 

15. Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni.  

16. Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku. 

17. Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda. 

18. Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa. 

19. Ama walio amini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za makaazi mazuri. Ndio pa kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda. 

20. Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni Motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mliyo kuwa mkiikanusha. 

21. Na tutawaonjesha adhabu khafifu kabla ya adhabu kubwa, huenda labda watarejea. 

22. Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi tutajilipiza kwa wakosefu. 

23. Hakika Sisi tulikwisha mpa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka kuwa kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili. 

24. Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu. 

25. Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye fafanua baina yao Siku ya Kiyama katika waliyo kuwa wakikhitalifiana. 

26. Je! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao, nao wanapita katika maskani zao hizo? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je, hawasikii? 

27. Je! Hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayo kula wanyama wao na wao wenyewe? Je! Hawaoni? 

28. Wanasema: Ushindi huu ni lini, kama mnasema kweli? 

29. Sema: Siku ya Ushindi, wale walio kufuru imani yao haitawafaa kitu, wala wao hawatapewa muhula. 

30. Basi wapuuze, nawe ngonja; hakika wao wanangoja. 

 

33 - AL-AH'ZAB

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. 

2. Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda. 

3. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa. 

4. Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia. 

5. Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 

6. Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha andikwa Kitabuni. 

7. Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu, 

8. Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu. 

9. Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda. 

10. Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali. 

11. Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali. 

12. Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao: Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu. 

13. Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu; hawakutaka ila kukimbia tu. 

14. Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu. 

15. Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa. 

16. Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu. 

17. Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. 

18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu. 

19. Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. 

20. Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu. 

21. Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana. 

22. Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu. 

23. Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo. 

24. Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 

25. Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza. 

26. Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka. 

27. Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. 

28. Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri. 

29. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa. 

30. Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.